Seneta Onyonka atangaza kifo cha mamake

Alielezea kwamba umauti ulimfika mamake wakati akipokea matibabu katika hospitali ya Aga Khan, jijini Nairobi

Marion Bosire
1 Min Read

Seneta wa kaunti ya Kisii Richard Momoima Onyonka, ametanga kifo cha mamake mzazi kilichotokea leo akiwa anaendelea kupokea matibabu hospitalini.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari Seneta Onyonka aliandika, “Ninasikitika kutangaza kifo cha mamangu mpendwa, Mama Teresia Nyaboke Omoke, aliyetuaga leo akiwa na umri wa miaka 81.”

Kiongozi huyo aliendelea kuelezea kwamba umauti umemfika mamake akipokea matibabu katika hospitali ya Aga Khan, jijini Nairobi.

Kulingana na taarifa hiyo, Mama Teresia Nyaboke Omoke alizaliwa Disemba 25, 1944, alikuwa mama aliyejitolea, nguzo ya familia na mwanamke aliyekuwa na imani, unyenyekevu na hekima.

Mama huyo anasemekana kuishi maisha yaliyojikita katika huduma, huruma na kujitoleakusikoyumba kwa familia yake na jamii.

“Kifo chake ni pigo kubwa sio tu kwa familia yetu lakini pia kwa wale wote ambao aligusa nyoyo zao kupitia kwaukarimu wake, maelekezo na upendo,” aliendelea kusema Onyonka katika taarifa huyo.

Kwa niaba ya familia yake, Seneta Onyonka alishukuru wote ambao wanaendelea kuwaombea, kuwatumia jumbe za faraja na misaada waliyopokea na watakayoendelea kupokea katika kipindi hiki kigumu.

“Tunaomba kwa unyenyekevu muendelee kutuombea tunapojaribu kukubaliana na msiba huu mkubwa,” alimalizia Onyonka akiahidi kutoa taarifa zaidi kuhusu mipango ya mazishi baadaye.

Share This Article