Huduma ya Taifa ya Polisi,NPS imeonya kuhusu uwezekano wa mafuriko katika maeneo zaidi ya 10 ya makazi jijini Nairobi huku mvua kubwa ikiendelea kusababisha usumbufu kote nchini.
Katika taarifa ya Aprili 29, 2026 NPS ilisema iko katika hali ya tahadhari pamoja na mashirika mengine ya serikali, kutokana na mvua inayoendelea ambayo imeongeza kwa kasi viwango vya maji katika njia kuu za maji.
“Ndani ya Nairobi, hali imezidi kuwa mbaya kutokana na kupanda kwa kasi kwa viwango vya maji katika mito mikuu, ikiwemo mito ya Nairobi, Mathare, Ngong, Kamiti na Athi,” ilisema taarifa ya NPS.
Mito yote hiyo huingia katika mfumo mkubwa wa Mto Athi, ambao kwa sasa una viwango vya maji vilivyo juu hatari kulingana na NPS.
Maeneo kadhaa yaliyo karibu na mito iliyotajwa yako katika hatari kubwa ya mafuriko, na wakazi wamehimizwa kuwa waangalifu. Maeneo yaliyo hatarini karibu na Mto Nairobi ni pamoja na Kileleshwa, Lang’ata, Ngara, Madaraka, Eastleigh na Kawangware.
Hatari ya mafuriko pia ni kubwa katika maeneo ya kusini mwa jiji kama vile Kibera na South C, yaliyo kando ya Mto Ngong.
Aidha, kuongezeka kwa viwango vya maji katika mito ya Kamiti na Athi kunatarajiwa kuathiri eneo la Kasarani, huku Mathare pia ikiathirika na mto wake.
Maeneo mengine yaliyo hatarini ni pamoja na Tatu City, Ruiru, Kitengela, Mlolongo na Syokimau karibu na Mto Athi.
Sehemu za katikati mwa jiji la Nairobi, Gikomba, Globe na Industrial Area zinakumbwa na hatari ya mafuriko kutokana na baadhi ya sehemu za Mto Nairobi kupita humo.
Kilimani, Westlands, Mukuru Kwa Reuben na Korogocho pia ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika.
Wakazi wa maeneo yanayokumbwa na mafuriko wanahimizwa kuhamia maeneo ya juu ikiwa watashauriwa kufanya hivyo, na kufuata maagizo ya uokoaji bila kuchelewa.
NPS imeushauri umma kuwa waangalifu sana wanaposafiri kutokana na barabara zilizojaa maji na mwonekano hafifu, hali inayoongeza kwa kiasi kikubwa hatari ya ajali.
Wakazi wanahimizwa kuepuka kutembea au kuendesha magari kwenye maji yanayotiririka, kwani hata maji yasiyo na kina kirefu yanaweza kuwa na nguvu ya kusababisha majeraha au uharibifu.