Waziri aliye na mamlaka makuu ambaye pia ni waziri wa mashauri ya nchi za kigeni Musalia Mudavadi amefurahikia ndoa ya mwanawe Michael na mpenzi wake Ann iliyofanyika jana hapa Nairobi.
Mudavadi amechapisha picha kadhaa za tukio hilo la kipekee na kuandika ujumbe mrefu wa shukrani kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.
“Leo moyo wangu umefurika na shukrani na furaha baada ya kushuhudia mwanangu Michael Lulu Mudavadi, akiungana katika ndoa na Ann Nixxie Nyaguthii Miitii,” alianza Mudavadi.
Aliendeleza ujumbe wake akiwazia jinsi mtu hupata hisia za kipekee kama baba wakati mwanawe anapiga hatua katika maisha yaliyojikita katika mapenzi, utu uzima, kujitolea na malengo.
Waziri huyo alisema siku ya jana haikuwa tu sherehe ya kufurahikia mioyo miwili ikiunganishwa na kuwa mmoja lakini pia ilikuwa siku ya kuunganishwa kwa familia mbili kwa upendo, heshima, imani na maadili mengine.
Mudavadi aliombea wanandoa hao wawili kwamba ndoa yao iwe na nguzo ya imani, itiwe nguvu na subira, ielekezwe na hekima na ijazwe na furaha ya kudumu.
“Michael na Ann, mnapoanza safari hii pamoja, naomba ndoa yenu iwe imejengwa katika imani daima, iimarishwe kwa uvumilivu, iongozwe na hekima, na ijazwe furaha ya kudumu,” aliandika Waziri Mudavadi.
Alimalizia kwa kutoa shukrani kwa marafiki, wageni waalikwa na wote walioungana nao kwa hafla hiyo muhimu.