EPRA yatangaza bei mpya za mafuta nchini

Kwenye taarifa siku ya Jumanne, EPRA iliongeza bei ya mafuta ya Petroli kwa shilingi 28.69 huku Dizeli ikipanda kwa shilingi 40.30 kwa kila lita, huku bei ya Mafuta taa ikisalia jinsi ilivyo.

Tom Mathinji
2 Min Read
EPRA yatangaza bei mpya za Mafuta.

Huku vita vya Mashariki ya Kati vikiendelea kutatiza usambazaji wa mafuta kote duniani, Halmashauri ya Kudhibiti Nishati na Kawi (EPRA), imefanyia mabadiliko bei za mafuta ambazo zitatumika katika muda wa mwezi mmoja ujao.

Kwenye taarifa siku ya Jumanne, EPRA iliongeza bei ya mafuta ya Petroli kwa shilingi 28.69 huku Dizeli ikipanda kwa shilingi 40.30 kwa kila lita, huku bei ya Mafuta taa ikisalia jinsi ilivyo.

Kulingana na EPRA,  Jijini Nairobi lita moja ya mafuta ya Petroli sasa inauzwa kwa shilingi 206 na centi 97 huku dizeli ikiuzwa kwa shilngi 206 na centi 84 wakati lita ya mafuta taa ikisalia kuuzwa kwa shilingi 152 na centi 78.

Jijini Mombasa lita ya moja ya Petroli inauzwa kwa shilingi 203 na centi 69 nayo Dizeli ikiuzwa kwa shilingi 203 na centi 56 huku lita moja ya ya Mafuta Taa ikiuzwa kwa shilingi 149 na centi  49.

Bei za juu zaidi zinatarajiwa Mandera ambako lita ya petrol itauzwa kwa shilingi 229 na centi 15 huku Dizeli ikiuzwa kwa shilingi 229 nayo mafuta taa shilingi  174 centi 96.

Na ili kuwakinga wakenya dhidi ya bei za juu zaidi za mafuta, EPRA ilisema ushuru wa bidhaa kwa mafuta ya petrol, dizeli na mafuta taa imepunguzwa kutoka asilimia 16 hadi asilimia 13.

EPRA ilidokeza kuwa ilichukua hatua hiyo baada ya kupanda kwa bei za mafuta katika soko la kimataifa.

Taarifa hiyo iliyotiwa saini na kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EPRA mhandisi Joseph Oketch, ilisema serikali imechukua hatua zaidi ya kuwakinga wakenya dhidi ya bei za juu, kwa kutumia shilingi bilioni 6.2 kutoka kwa matozo ya ustawi ya bidhaa ya petrol kuhakikisha udhabiti wa bei za mafuta.

Share This Article