Rais William Ruto kesho Alhamisi anatarajiwa kuzindua awamu ya 2B na 2C ya ujenzi wa reli ya SGR.
Uzinduzi huo utafanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Walimu cha Narok.
Awamu ya 2B inahusisha ujenzi wa SGR kutoka mjini Naivasha hadi Kisumu.
Kwa upande mwingine, awamu ya 2C inahusisha ujenzi wa reli hiyo kutoka mji wa Kisumu hadi mji wa mpakani wa Malaba katika kaunti ya Busia.
Kimsingi, ujenzi wa reli hiyo uliosubiriwa kwa hamu na ghamu utaunganisha miji ya Naivasha, Kisumu na Malaba.
Nao unatarajiwa kupiga jeki kwa kiwango kikubwa usafiri kuelekea magharibi mwa nchi, na wakati huo huo kufungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wakazi wa maeneo ambako reli hiyo itapitia.
“Sisi kama kaunti ya Narok tumefurahia mno mradi huu kwa sababu kwanza kabisa utabuni nafasi za ajira kwa watu wetu, kutakuwa na kazi nyingi itakayofanywa na pia usafiri kati ya hapa na Nairobi, watu wetu watakuwa wakitumia reli kutoka hapa hadi Nairobi,” amesema Patrick Ole Ntutu, Gavana wa kaunti ya Narok.
Matamshi sawia yametolewa na Gavana wa Kisumu, Prof. Peter Anyang’ Nyong’o.
“Kwa kaunti ya Kisumu, athari za mradi huu ni kubwa mno. Reli hii itapanua biashara, kupunguza gharama ya kufanya biashara, kuchochea ustawi wa viwanda, kuimarisha mitungo yetu ya kilimo cha thamani, na kuchochea uwekezaji mpya katika utunzaji vitu kwenye ghala, ujenzi, uvuvi na uzalishaji,” amesema Prof. Nyong’o.
Ujenzi wa reli hiyo ulikusudiwa kuanza mwezi Januari mwaka huo lakini hilo halikutimia.
Kisha Rais Ruto alinukuliwa akisema ujenzi huo utaanza mwezi Februari lakini pia hilo halikutimia yamkini kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo changamoto za kifedha.
Waziri wa Barabara Davis Chirchir amenukuliwa akisema ujenzi wa reli hiyo unatarajiwa kuchukua kipindi cha miaka mitatu.
Awamu ya kwanza ilihusisha ujenzi wa reli ya SGR kutoka Mombasa hadi Nairobi na kisha Nairobi hadi Naivasha.