Afisi ya waziri aliye na mamlaka makuu imethibitisha kwamba wadhifa huo wa Musalia Mudavadi umelindwa na unawiana na makubaliano yaliyotiwa saini kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 kati ya vyama tanzu vya muungano wa Kenya Kwanza.
Katika taarifa kwa umma iliyotolewa Jumamosi Machi 15, 2025, afisi hiyo ilifafanua kwamba muunganisho wa hivi maajuzi kati ya chama cha Amani National Congress (ANC) na kile cha United Democratic Alliance (UDA) hauathiri jukumu la Mudavadi serikalini.
Ufafanuzi huu unajiri wakati ambapo kumekuwa na uvumi kuhusu wadhifa wa awali wa Mudavadi kama kiongozi wa chama cha ANC huku miungano mingine ya kisiasa ikiendelea kushuhudiwa.
Kulingana na afisi ya waziri aliye na mamlaka makuu, serikali ya Kenya Kwanza imejitolea kwa jukumu lake asilia hata baada ya makubaliano ya hivi maajuzi kati ya UDA, Keny Kwanza na ODM.
Taarifa hiyo ilitoa hakikisho kwa umma kwamba baada ya muunganisho huo kuidhinishwa rasmi, serikali ya Kenya Kwanza inaangazia kutekeleza ahadi ilizotoa kwa wakenya na kudumisha utulivu wa kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.
Kitengo cha mawasiliano cha afisi hiyo ya Mudavadi kilitambua pia wadau muhimu hasa waliokuwa wafuasi na wanachama wa chama cha ANC waliofanikisha mabadiliko.
Kilisema kwamba muunganisho huo ni hatua muhimu katika kuimarisha hata zaidi serikali ya Kenya Kwanza.