Kundi la wanasayansi wa kike wa chuo kikuu cha Nairobi – UoN, waliadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake na wasichana katika sayansi katika shule ya upili ya wasichana ya Ole Tipis katika kaunti ya Narok.
Wakiongozwa na Dkt. Esther Kanduma, wanawake hao waliadhimisha miaka kumi ya maendeleo ya teknolojia chini ya maudhui “Kuchambua kazi za STEM: Sauti ya mwanamke katika sayansi”.
“Kwa sasa ni asilimia 30 tu ya wanawake walio katika kazi zinazohusiana na sayansi.” alisema Kanduma huku akihimiza wadau kusaidia mipango ya kuhakikisha uwakilishi sawa wa kijinsia katika nyanja ya Sayansi, Teknolojia na Hisabati.
Alielezea kwamba mchakato wa uhamasicho unalenga kuchochea wanawake na wasichana na kutoa ufahamu kuhusu fursa za kazi zilizo katika nyanja ya Sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati almaarufu STEM.
Mwalimu mkuu wa shule ya Ole Tipis Bi. Ololokula, alipongeza mpango huo kwa kuboresha matokeo ya shule hiyo katika Sayansi na kumotisha wanafunzi.
“Wasichana wanaweza kukuzwa kuwa wanasayansi wa siku za usoni.” Alisema mwalimu huyo akiongeza kwamba wasichana 10 walipata alama ya A- katika mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne KCSE wa mwaka jana.
Kulingana naye, wengi wa wasichana hao waliofanya vyema walishiriki mpango huo wa uhamasisho ambao anasema umechangia wasichana wengi kujiunga na vyuo vikuu vya umma.
Profesa Esther Maina, mjuzi wa kemia hai katika chuo kikuu cha Nairobi na mwanachama wa bodi ya usimamizi ya shule ya Ole Tipis alisema shule hiyo ndiyo ilitangulia kunufaika na mpango huo ulioanzishwa mwaka 2019.
Alisisitiza kuhusu umuhimu wa kutayarisha wasichana kwa kazi za Sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati kwani sayansi na teknolojia ni muhimu kwa siku zijazo.