Watu maarufu wadaiwa kulipa waathiriwa wa P Diddy ili wanyamaze

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Marekani Ray J amesema kwamba watu fulani maarufu wamewasiliana naye wakiwa na woga kutokana na uhusiano kati yao na Diddy.

Kulingana naye, watu hao maarufu sasa wanatafuta waathiriwa wa sherehe za ngono zilizokuwa zikiandaliwa na Diddy na kuwalipa ili wanyamaze.

Ray ni mmoja wa waliohojiwa katika filamu ya matukio halisi ya TMZ iitwayo “The Downfall of Diddy: Inside the Freak-Offs” na anasema watu maarufu wanajaribu sana kuzuia waathiriwa hao kabla yao kuwasilisha kesi mahakamani kudai fidia.

Wakili Tony Buzbee ambaye anawakilisha waathiriwa wa Diddy zaidi ya 100, naye aliibua madai sawia.

Buzbee ambaye pia anaangaziwa kwenye filamu hiyo, anasema alituma barua ya mahitaji kwa baadhi ya watu hao maarufu akiwataka wafidie waathiriwa au wakabiliwe na kesi.

Katika filamu hiyo, Ray anaonekana mwenye woga huku akisimulia jinsi watu hao maarufu waliwasiliana naye.

Maafisa wa polisi walipekua nyumba ya Diddy kabla ya kukamatwa kwake na inaripotiwa kwamba walitwaa video za sherehe hizo alizokuwa akiandaa na kwamba baadhi ya watu maarufu nchini Marekani wamenakiliwa humo.

Huku haya yakijiri, Ray J alisema kupitia akaunti yake ya Instagram kwamba mtu alijaribu kumfyatulia risasi ila hakutoa maelezo ya kina.

Awali alisema alikutana na wanawe Diddy kwenye sherehe ya Halloween na walionekana kana kwamba walitaka kumpiga kutokana na matamshi yake kuhusu baba yao.

Diddy anazuiliwa katika gereza la Brooklyn kufuatia madai kadhaa yanayohuasiana na ulanguzi wa watu ili kuwatumia kingono.

Share This Article