Wakenya wamejitokeza kwa wingi katika miji mbalimbali nchini kushiriki maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024.
Maandamano hayo yanahudhuriwa hasa na vijana wanaofahamika mno kama Gen Z.
Wengi wao wamejitokeza kushiriki maandamano hayo katika miji mbalimbali kama vile Nairobi, Mombasa, Kisumu, Kakamega, Nakuru, Eldoret na Nyamira miongoni mwa mingine.
Jijini Nairobi, usalama umeimarishwa huku maafisa wa usalama wakishika doria wakati waandamanaji wakijitokeza asubuhi na mapema kupaza sauti za kupinga mswada huo.
Majengo muhimu kama vile bunge na Jumba la Mikutano ya Kimataifa la Kenyatta, KICC yamezingirwa na polisi. Baadhi ya barabara pia zimefungwa.
Waandamanaji wameonekana wakibeba mabango ya kupinga Mswada wa Fedha 2024 na kulalamikia hali ngumu ya maisha nchini.
Wametoa wito kwa wabunge kukatalia mbali mswada huo wanaodai utafanya gharama ya maisha kupanda zaidi.
Wabunge wanatarajiwa kupiga kura ya ama kupitisha au kukatalia mbali mswada huo leo Jumanne.