Dkt. Ezekiel Mutua ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Hakimiliki za Muziki Nchini Kenya, MCSK amezungumza baada ya kulaumiwa na bodi inayosimamia hakimiliki nchini kwa kutogawa mirabaha inavyofaa.
Bodi hiyo ya hakimiliki, KECOBO iliandika waraka kwa tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC, kuiomba ichunguze MCSK kwa kile ilichokitaja kuwa matumizi mabaya ya shilingi milioni 56, pesa ilizokusanya kwa niaba ya wasanii kama mirabaha.
Mutua sasa anasema kwamba walitangaza wazi zoezi la kugawa pesa hizo kwa wasanii husika kupitia tangazo la gazeti Januari 19, 2024 ambapo walitaja kiasi cha pesa zitakazogawiwa wasanii na mtindo utakaotumika kuzigawa.
Mchakato mzima kulingana naye ulikuwa uanze Januari 25 na utakamilika Machi 29, 2024.
Anaelezea kwamba watatumia kumbukumbu za muziki uliochezwa kutoka kwa vyombo vya habari mbalimbali kugawa pesa hizo.
Mutua anashangaa kwamba bodi ya hakimiliki inazungumzia sheria ya asilimia 70 ambayo kulingana naye haiko kwenye sheria ya hakimiliki au katiba ya Kenya.
“Ni kama wamekosa mawazo sasa. Mtu aje anionyeshe sehemu ya sheria inayozungumzia sheria ya asilimia 70,” aliandika Mutua huku akishangaa fedha zaidi ambazo KECOBO inahisi zingesambaziwa wasanii zingetoka wapi ilhali mwaka 2023, kiwango cha uchezaji wa muziki wa Kenya kilikuwa asilimia 10 pekee.
Mutua anashangaa pia ni kwa nini KECOBO inatoa maelezo mengi hata baada ya kuitisha uchunguzi.
Amesema mashirika ya usimamizi jumla ambayo yanahusika na mirabaha ni ya kibinafsi na hayafadhiliwi na serikali.
“Serikali haifadhili uaandaaji wa muziki. Wasanii wataamua hatima yao. Hatima hiyo sio serikali kuendesha shughuli za makundi ya usimamizi jumla,” amesema Mutua.