Wanachama wa kamati kuu ya kaunti ya Nandi ambayo ni sawa na baraza la mawaziri katika serikali kuu wameapishwa.
Watendakazi hao wa kaunti walisailiwa yapata wiki moja iliyopita.
Mahakama ya kuu mjini Eldoret ilitupilia mbali uteuzi wa wanachama wa kamati kuu ya kaunti kufuatia kesi iliyowasilishwa na mkazi mmoja wa kaunti hiyo Novemba mwaka jana.
Onesmus Kimeli alipinga uteuzi wa wanachama wa kamati kuu kwa misingi kwamba uteuzi wao haukuzingatia sheria ya thuluthi mbili ya uwakilishi wa kijinsia.
Kufuatia hilo, bunge la kaunti ya Nandi liliidhinisha uteuzi wa wanachama watatu tu wa kamati kuu ya kaunti Novemba 14 2022.
Kesi hiyo iliamuliwa Oktoba 18, 2023 ambapo uteuzi wa Kiplimo Lagat, Phillomena Kiptoo, Ruth Koech, Kibet Ronoh, Alfred Lagat, Hillary Serem, Isiah Keter na Scholastica Tuwei, ulitupiliwa mbali.
Gavana Stephen Sang alilazimika kuteua upya wanachama wa kamati hiyo kuu na kuwasilisha majina yao bungeni mchakato ambao umeishia uapisho.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuapisha wanachama hao, Gavana Sang aliwapongeza huku akisema kwamba sasa wanaangazia kazi ya kuhakikisha kukamilishwa kwa miradi.