Serikali imezindua zoezi la usaili wa kitaifa wa watengenezaji wa pombe.
Katibu katika wizara ya usalama wa taifa Dkt. Raymond Omollo, alisema kundi maalum la asasi mbali mbali limebuniwa ili kuongoza mchakato huo.
Kupitia kwa taarifa Omollo alidokeza kuwa leseni zote za viwanda na watengenezaji wa pombe zimefutiliwa mbali, hadi kukamilika kwa shughuli hiyo.
“Tunalenga watengenezaji mvinyo, huku maeneo 29 yakifanyiwa uchunguzi. Hadi sasa tumegundua kuwa leseni za kampuni 35 zilikuwa zimefutiliwa mbali awali au hazikuwa zikitumika,” alisema Omollo.
Usaili huo ulitokana na agizo la serikali la March 6, 2024, lilipo tangaza vita dhidi ya utengenezaji, utumizi na usambazaji wa pombe haramu na mihadarati kote nchini.
Omollo alibainisha kuwa shughuli hiyo inawalazimu watengenezaji wa pombe kuweka maabara ya kudhibiti ubora wa bidhaa ambayo yana vifaa maalum na wafanyakazi walio na ujuzi na kuhakikisha uchunguzi wa kina wa malighafi na bidhaa zilizomalizwa kutengenezwa.