Mifugo zaidi ya 700 waibwa Isiolo na Samburu

Tom Mathinji
1 Min Read
Zaidi ya mifugo 700 waibwa kaunti ya Isiolo.

Idadi isiyojulikana ya majambazi waliwapiga risasi na kuwaua watu watatu na kuwajeruhi wengine watano, huku zaidi ya mifugo 700 wakiibwa katika visa tofauti vya ujangili kaunti za Isiolo na Samburu.

Mashambulizi hayo yaliripotiwa Samburu Mashariki, Bojidare na Hola Bule katika kaunti ya Isiolo.

Katika shambulizi la Bojidare, majangili walivamia manyatta na kupiga risasi kiholela na kuwaua watu wawili papo hapo na kuwajeruhi watatu, kabla ya kuiba ng’ombe 250 na mbuzi 300.

Hata hivyo kulingana na huduma ya taifa ya polisi kupitia mtandao wa X, maafisa wa polisi walisema walipata mbuzi 300 na ng’ombe 30 walioibwa katika kisa hicho.

Katika tukio la pili, majangali wanadaiwa kushambulia eneo la Hola Bule na kuiba ng’ombe 19.

Huduma ya taifa ya polisi ilisema wakati wa uvamizi huo, mtu mmoja aliuawa huku wawili wakijeruhiwa akiwemo afisa wa akiba wa polisi.

Na katika tukio la wizi wa mifugo kaunti ya Samburu, majangili wawili waliuawa katika mto Waso huku mifugo 211 waliokuwa wameibwa wakipatikana Samburu Mashariki.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article