Bodi ya Dawa na Sumu humu Nchini, PPB imeonya umma dhidi ya matumizi ya bidhaa kwa jina “Yoni Pearls” ambazo huaminika kusaidia kutoa uchafu katika uke.
Kupitia taarifa, bodi hiyo ilisema kwamba “Yoni Pearls” hazijasajiliwa wala kuidhinishwa kwa matumizi nchini Kenya kulingana na sheria ya dawa na sumu.
Ilielezea kwamba matumizi ya bidhaa hiyo yanahatarisha afya ya umma kwani bodi hiyo haiwezi kuthibitisha ubora, usalama na ufanisi wake.
PPB imeonya vikali dhidi ya usambazaji, uuzaji na matumizi ya bidhaa hiyo au nyingine za matumizi sawia.
Wahudumu wa afya humu nchini wameombwa wawe wakitoa ripoti kwa bodi ya dawa na sumu kuhusu bidhaa na vifaa vinavyoshukiwa.
Bidhaa hiyo imejipatia umaarufu kati ya kina dada humu nchini kwa madai kwamba inatibu maradhi mengi ya njia ya uzazi kwa miili ya wanawake.