Rais wa China Xi Jinping amesema China na Urusi zinapaswa kuimarisha uhusiano wao ili kufufua uchumi wa mataifa hayo.
Akizungumza wakati wa ziara ya Rais Vladimir Putin nchini humo, Xi alipongeza uhusiano kati ya nchi hizo mbili akisema umefanikiwa kuboresha ushirikiano wao wa kisiasa.
Kuhusu vita vya Mashariki ya Kati, Rais Xi alisema wakati umewadia wa kumaliza mgogoro huo na kutoa fursa kwa hali ya utulivu na amani kupatikana.
China imesema ndiye mnunuzi mkubwa wa mafuta kutoka Urusi na pia mshirika wake mkuu wa kibiashara, hasa baada ya mataifa ya Magharibi kukata uhusiano wa kiuchumi na Urusi kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine.
Kwa upande wake, Rais Putin alisema uhusiano kati ya Urusi na China ni wa kiwango cha juu na umechukua mkondo unaofaa.
Kwenye hotuba yake, hakusita kuipigia debe Urusi akiitaja kama muuzaji wa nishati anayeaminika licha ya vita vinavyoshuhudiwa Mashariki ya Kati.
Kwenye ziara hiyo, Rais Putin ameandamana na ujumbe mkubwa unaojumuisha viongozi wa serikali na wafanyabiashara wa Urusi.