Wizara ya Kilimo imeweka mikakati kuhakikisha uzalishaji wa mchele unaongezeka hapa nchini na kupunguza uagizaji zao hilo kutoka nje.
Kulingana na wizara hiyo, taifa huhitaji metriki tani milioni 1.1 za mchele, lakini lina uwezo wa kuzalisha metrik tani 300,000 pekee.
Katibu katika Wizara ya Kilimo Dkt. Kiprono Ronoh leo Jumanne, amesema kwa ushirikiano na shirika la utafiti wa kilimo na mifugo KALRO, wizara yake imeanzisha mpango wa ukuzaji aina ya mchele katika nyanda za juu na nyanda za chini, akidokeza kuwa aina hiyo ya mchele hukuzwa sawia na mahindi na haihitaji unyunyizaji wa maji.
“Tumewasambazia wakulima mbegu ya aina hiyo ya mchele, ili kuongeza uzalishaji. Kufikia mwaka 2027, tunalenga kuafikia uzalishaji wa metrik tani 800 za mchele,” alisema Dkt. Ronoh katika mahojiano na shirika la utangazaji nchini KBC.
Dkt. Ronoh alisema Kenya itanawiri bila kuagiza chakula kutoka nje, kupitia miradi kadhaa iliyoanzishwa kushughulikia upungufu wa mchele.
Kulingana na katibu huyo, miradi hiyo inatekelezwa Ahero, Galana Kulalu, Mwea na Taita Taveta, kupiga jeki uzalishaji mchele.
“Tumeanzisha miradi kadhaa kushughulikia upungufu wa mchele hapa nchini. Juma lililopita tulifungua mpango wa unyunyiziaji mashamba maji katika shamba la mpunga la ekari 20,000 kaunti ya Migori,” alisema Dkt. Ronoh.