Wetang’ula: Maandamano ya Jumatano yatakuwa ya amani

Tom Mathinji
2 Min Read
Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang'ula (Kulia) na Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini Mark Dillard.

Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula, ametoa wito kwa wanaoandaa maandamano Jumatano Juni 25,2025, kuyashiriki kwa amani ili kuepusha kupoteza maisha na mali.

Akizungumza alipokuwa mwenyeji wa balozi wa Marekani anayeondoka Mark Dillard aliyetaka kufahamishwa mipango ya Bunge kuhusu mchecheto uliopo, Wetang’ula alisema matarajio yake ni kwamba maandamano hayo yatakuwa ya amani.

“Iwapo maandamano hayo yatakuwa ya amani, basi hakutakuwa na wasiwasi wowote, bunge liko tayari kushughulikia maswala hayo, lakini iwapo maandamano yatageuka na kuwa vurugu, basi bunge halitakuwa na uwezo kuyashughulikia, ila asasi zingine zitaingilia kati, lakini natumai yatakuwa ya amani,” alisema Wetang’ula

Balozi Dillard kwa upande wake alielezea wasiwasi kuhusu kile alichokitaja kuwa utumizi wa nguvu kupita kiasi, na mauaji ya mwanablogu  Albert Ojwang alipokuwa kwenye korokoro za polisi.

“Tuko makini kuhusu uwajibikaji, kuhakikisha polisi wanawajibishwa huku tukitarajia makumbusho hayo ya kesho yatakuwa ya amani,” alidokeza balozi Dillard said.

Aidha Spika Wetang’ula alirejelea ujumbe wake wa hapo awali kwamba maafisa wachache wasio na maadili, hawapaswi kuchafua jina la kikosi kizima cha polisi.

“Polisi hufanya kazi nzuri ya kulinda maisha na mali, ukosefu wao husababisha vurugu. Lakini kama kuna maafisa ambao ni watundu wanapaswa kushughulikiwa binafsi wanapopatikana na hatia,” alisema Wetang’ula.

Aliongeza kuwa maandamano huwa na nia njema, akini wahuni na wakora wanapoingilia na kuanza kuwapora wafanyabiashara na kuiba mali, basi maandamano hayo hugeuka na kuwa shughuli za uhalifu,” alidokeza Spika huyo.

Website |  + posts
Share This Article