Wizara ya Afya imethibitisha visa vinne vipya vya ugonjwa wa Ebola kutoka kwa wagonjwa walio kwenye karantini kufutia kisa cha kwanza kilichoripotiwa mapema mwezi huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyoandikwa na Mkurugenzi wa huduma za matibabu Dkt.Patrick Amoth visa hivyo vinne vimebainika baada ya wagonjwa hao kufanyiwa vipimo katika maabara ya kitaifa ya virusi na yale ya taasisi ya utafiti wa matibabu nchini (KEMRI).
Wagonjwa hao wanne wanafikisha jumla ya visa saba vilivyoripotiwa nchini vya ugonjwa wa Ebola unaosababishwa na virusi vya Bundiburgyo
Kulingana na Amoth mgonjwa mmoja aliyepatikana na virusi hivyo mwanaume aliyekuwa na uhusiano wa karibu na mwanaume wa kwanza aliyefariki.
Visa vingine vitatu vipya vinajumuisha wahudumu wa afya wakiwemo wanaume wawili na mwanamke mmoja waliomhudumia marehemu alipowasilishwa katika hospitali ya Nairobi.
Maafisa hao wa matibabu wana umri wa miaka 29,35 na 32 na walianza kuwa na dalili za Ebola, wakiwa wametengwa na tayari wamehamishiwa katika vituo maaluma vya kupokea matibabu.
Wizara ya afya imesema watu 128 kati 130 ikiwemo familia ya mgonjwa wa kwanza aliyefariki wamejitenga kwa siku 21 .