Wasanii wa muziki wa Bongo Flava nchini Tanzania Whozu, Billnass na Mbosso wamepata afueni baada ya adhabu ya kuwafungia kujihusisha na sanaa kuondolewa.
Baraza la Sanaa la Taifa – BASATA lilikuwa limeadhibu watatu hao kutokana na video ya wimbo wao iliyochukuliwa kama iliyokiuka maadili ya kijamii.
Whozu kama mwenye wimbo alipigwa marufuku ya kujihusisha na usanii kwa muda wa miezi 6, akatozwa faini ya shilingi milioni 3 na kutakiwa aondoe video hiyo mitandaoni.
Mbosso na Billnass ambao walihusishwa kwenye wimbo huo walitozwa faini ya shingili milioni 3 na kufungiwa kwa miezi mitatu kila mmoja.
Wasanii hao walikata rufaa na leo kikao cha kusikiliza rufaa hiyo kikaandaliwa katika afisi za uwanja wa michezo wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam, chini ya uongozi wa Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro na Naibu wake Hamis Mwinjuma maarufu Mwana FA.
Kikao hicho kiliafikia suluhisho la kuondolea wasanii wote marufuku ya kujihusisha na kazi za usanii na badala yake wakatakiwa walipe tu faini.
Viwango vya faini vilifanyiwa marekebisho ambapo Whozu anafaa kulipa faini ya shilingi milioni 5 pesa za Tanzania, Billnass Milioni moja na Mbosso milioni tatu
Whozu ametakiwa kuhakikisha kwamba video ya wimbo huo kwa jina “Ameyatimba” haipatikani mitandaoni.
Watatu hao wako huru kurejelea kazi punde baada ya kulipa faini.
Waziri Ndumbaro amesihi wasanii nchini Tanzania kuzingatia maelekezo ya maadili wanapoonyesha ubunifu wao kulingana na mwongozo wa BASATA.