Wezi wa mifugo wauawa eneo la Karare Saku, Marsabit

Wako Ali
1 Min Read

Wezi watatu wa mifugo wameuawa baada ya jaribio lao la wizi wa mifugo kutibuka.

Watatu hao waliuawa na polisi eneo la Kituruni, wadi ya Karare baada ya majibizano makali ya risasi na maafisa wa usalama waliokuwa wakiwafuata.

Aidha, wezi wengine waliokuwa wamejihami kwa bunduki walifanikiwa kutoroka.

Kamanda wa kaunti ya Marsabit Leonard Kimaiyo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Jumanne.

Kimaiyo ameongeza kuwa bunduki mbili zilipatikana kutoka kwa wezi hao, moja aina ya AK-47 na nyingine aina ya G3.

Kulingana na kamanda huyo, wakazi wa eneo hilo wanasema huenda wezi hao walitotokea kaunti jirani ya Samburu.

Awali, wezi hao walivamia eneo la Shrine nje ya mji wa Marsabit ambako jaribio la wizi wa mifugo lilitibuka.

Kamanda Kimaiyo ametoa onyo kali kwa wezi wa mifugo akisema serikali itakabiliana nao vilivyo.

Polisi wameimarisha msako dhidi ya wezi waliotoroka.

Wako Ali
+ posts
TAGGED:
Share This Article