Spika wa bunge la taifa Moses Wetang’ula, ametoa wito kwa viongozi kuhakikisha matamshi na matendo yao yanakuza umoja wa Wakenya.
Wetang’ula alisisitiza kuwa viongozi hasa walio katika ngazi ya kitaifa, wanapaswa kuwa makini kuhakikisha hawasababishi migawanyiko kwa manufaa ya maeneo fulani.
Kulingana na spika huyo, wale wanaojihusisha na migawanyiko hiyo hawapaswi kushikilia nyadhifa na wanapaswa kufurushwa uongozini.
“Tunataka kuwa na viongozi ambao wanajua kiwango wanachopaswa kufika, kile anachosema, mahali pa kuyasema, jinsi ya kuyasema na athari za matamshi hayo katika jamii. Na kama kuna mtu yeyote ambaye anataka kuvuruga amani ya nchi, atolewe kwa sababu tunataka amani,” alisema Wetang’ula.
Huku akiashiria mipango inayoendelea ya kumfurusha Naibu Rais Rigathi Gachagua kutokana na mienendo yake, Wetang’ula alisema Wakenya wote wana fursa sawa, licha ya wanakotoka.
“Nawahimiza viongozi kuepuka siasa zinazosababisha migawanyiko ya kikabila na kimaeneo. Katiba inatoa fursa kwa kila mkenya kuishi, kumiliki mali na kufurahia amani popote hapa nchini.”
Wakati huo huo, Wetang’ula alitoa wito kwa viongozi wote kuheshimu afisi ya rais
“Kwa sasa kuna serikali moja inayoongozwa na Rais William Ruto,” alisema spika huyo alipohudhuria ibada ya Jumapili katika kanisa katoliki la St. John Wamunyu, kaunti ya Machakos.