Rais Ruto: Serikali jumuishi imefanikisha ustawi wa maendeleo

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais William Ruto asema serikali jumuishi imefanikisha ukuaji wa uchumi.

Rais William Ruto amesema kubuniwa kwa serikali jumuishi kumefanikisha kupiga jeki ustawi wa kijamii na kiuchumi wa taifa hili, huku miradi kadhaa ya maendeleo ikitekelezwa.

Akizungumza Alhamisi alipoanza ziara ya siku nne katika eneo la Nyanza, kabla ya sherehe za Madaraka tarehe mosi mwezi Juni, kiongozi wa taifa alielezea umuhimu wa juhudi za pamoja ili kufanikisha ujenzi wa taifa.

“Tumeweka pamoja juhudi kuwaunganisha wakenya. Lazima tuangamize siasa za migawanyiko ambazo zinahatarisha taifa hili,” alisema Rais Ruto.

Akiwa ameandamana na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, Rais Ruto alikagua ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika mtaa wa Lumumba mjini Kisumu, uliozinduliwa mwezi Agosti mwaka 2024.

Rais Ruto azindua uwekaji lami wa barabara ya kilomita 40 ya Marindi-Oria Bridge katika eneo la Ndhiwa, kaunti ya Homa Bay.

“Tumeridhishwa na hatua zilizopigwa katika ujenzi wa nyumba 2,384 ambao umewaajiri mamia ya vijana,” alidokeza Rais Ruto.

Awali kiongozi wa taifa alizindua uwekaji lami wa barabara ya kilomita 40 ya Marindi-Oria Bridge katika eneo la Ndhiwa, kaunti ya Homa Bay.

“Barabara hii itapiga jeki kilimo, uvuvi na kilimo cha majini, kando na kuchochea uzalishaji bidhaa katika eneo hilo,” aliongeza Rais Ruto.

Ziara yake itakamilika siku ya Jumapili ambapo ataongoza taifa katika sherehe za mwaka huu za Madaraka, zitakazoandaliwa chini ya kauli mbiu ‘ Uchumi Samawati na Masuala ya Bahari’ katika uwanja wa Raila Odinga, kaunti ya Homa Bay.

Website |  + posts
Share This Article