Spika wa bunge la taifa Moses Wetang’ula ametetea sheria ya matumizi mabaya ya kompyuta na uhalifu wa mtandaoni ya mwaka 2025 akisema kwamba inalenga kulinda familia.
Akizungumza wakati wa ibada katika kanisa Katoliki la Mtakatifu Teresa Isanjiro mjini Malava, kaunti ya Kakamega, Wetang’ula alipuuzilia mbali madai kwamba sheria hiyo inalenga kuhujumu uhuru wa kujieleza.
Badala yake, alielezea kwamba inalenga kulinda watoto ambao wanapatana na maudhui yasiyowafaa mitandaoni.
Wetang’ula aliongeza kwamba sheria hiyo inalenga kuhimiza uwajibikaji mitandaoni huku ikipambana na itikadi kali, unyanyasaji mitandaoni na uenezaji wa mafunzo mabaya ya kidini nchini Kenya.
Kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichung’wah ambaye alikuwa ameandamana na Wetang’ula katika hafla hiyo, naye pia alitetea sheria hiyo akisema kumekuwa na usambazaji wa habari zisizo sahihi kuhusu lengo la sheria hiyo.
Haya yanajiri wakati ambapo mahakama imesitisha utekelezaji wa sheria hiyo ambayo ilitiwa saini na Rais William Ruto Oktoba 15, 2025 pamoja na sheria nyingine 7 ikiwemo ya ubinafsishaji wa mali ya umma.
Jaji Lawrence Mugambi wa Mahakama Kuu ya Nairobi alitoa maagizo ya kusimamisha utekelezaji huo Oktoba 22 kufuatia ombi lililowasilishwa na Reuben Kigame na Tume ya Kutetea Haki za Binadamu nchini, KHRC.
