Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula anaongoza ujumbe wa wabunge wa Kenya kuhudhuria Maombi ya Taifa ya kila Mwaka yatakayoandaliwa jijini Washington nchini Marekani.
Maombi hayo huwaleta pamoja viongozi zaidi ya 3,500 kutoka kote duniani na yamepangwa na shirika la “The Fellowship Foundation.”
Aidha, maombi hayo yalianzishwa na Rais wa zamani wa Marekani Dwight D. Eisenhower mnamo mwaka 1953 na huwaleta pamoja viongozi wa kisiasa, kijeshi, biashara na mashirika ya kijamii.
Ujumbe wa Kenya unajumuisha kiranja wa wengi Silvanus Osoro na wabunge Beatrice Elachi (Dagoretti Kaskazini), Julius Melly (Tinderet), Chege Kiragu (Limuru) na Seneta Dan Maanzo (Makueni).
Wabunge hao watakuwa wenyeji wa wenzao kutoka Bunge la Marekani.
Punde baada ya kuwasili jijini Washington, ujumbe huo ulilakiwa na Balozi wa Kenya nchini Marekani David Kerich.
Ingawa masuala ya kidini yanasalia nguzo muhimu ya hafla hiyo, maombi hayo pia utumiwa kukuza ushirikiano wa kimakakati miongoni mwa washiriki.
