Waziri Wahome atoa onyo kali kwa wanyakuzi wa ardhi ya umma

Martin Mwanje
1 Min Read

Waziri wa Ardhi Alice Wahome ametoa onyo kali kwa watu walionyakua ardhi ya umma. 

Anaonya kuwa wizara yake itashirikiana na kitengo cha upelelezi wa jinai, DCI na tume ya kupambana na ufisadi, EACC kuhakikisha ardhi yote ya umma iliyonyakuliwa inarejeshwa.

Aliyasema hayo alipofanya ziara ya kushtukiza katika sajili ya ardhi ya kaunti ya Kilifi leo Jumatatu.

Ziara hiyo ilinuia kutathmini mazingira ya utendakazi na vizuizi kwa utoaji mufti wa huduma kwa raia.

Waziri Wahome aidha ameapa kulainisha mchakato wa kuwafidia wamiliki wa ardhi na mali walioathiriwa na Ukanda Maalum wa Kiuchumi wa Dongo Kundu jijini Mombasa kufuatia maagizo makali yaliyotolewa na Rais William Ruto.

Aliongeza kuwa operesheni ya kuwafurusha walaghai wanaotarajia kulipwa fidia inaendelea ili kuhakikisha kuwepo kwa orodha sahihi ya watakaofaidika.

Rais William Ruto ametangaza vita vikali dhidi ya watu walionyakua ardhi ya umma na kuapa kuhakikisha inarejeshwa.

Siku chache zilizopita, serikali ilianza ubomozi wa nyumba zilizojengwa kwenye ardhi ya kampuni ya East African Portland Cement na kuonya walionyakua ardhi ya umma kuwa hivi karibuni watakiona cha mtema kuni.

 

Share This Article