Waziri wa Ulinzi wa Ukraine awasili Korea Kusini kuzungumzia silaha

Martin Mwanje
1 Min Read
Rustem Umerov - Waziri wa Ulinzi wa Ukraine

Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Rustem Umerov amewasili nchini Korea Kusini na anafanya mikutano ya pande mbili.

Haya yamesemwa na Ukraine kufuatia ripoti kuwa maafisa kutoka nchi hizo mbili watazungumzia msaada wa kijeshi unaoweza kutolewa na Korea Kusini kwa Ukraine.

Ziara hiyo inakuja wakati Korea Kusini imeashiria kuwa inaweza ikabatilisha sera ya muda mrefu ya kutotoa silaha kwa nchi zilizopo kwenye mgogoro.

Hatua hiyo ilifuatia ufichuzi kuwa Korea Kaskazini imepeleka maelfu ya wanajeshi wake kusaidia juhudi za kivita za Urusi dhidi ya Ukraine.

Wizara ya Ulinzi ya Ukraine imeithitishia AFP kuwa Umerov tayari yupo nchini Korea Kusini na kwamba “mikutano yake huko inafanyika”.

Vyombo vya habari vya Korea Kusini vilikuwa vimeripoti juu ya mkutano uliopangwa kufanyika kati ya Umerov na Rais Yoon Suk Yeol — ingawa Ofisi ya Rais ilikataa kuthibitisha hilo.

Ujumbe wa Ukraine ulitarajiwa “kutoa taarifa za kijasusi juu ya upelekwaji wa wanajeshi wa Korea Kaskazini nchini Urusi” na kutafuta msaada wa Korea Kusini kwa ajili ya juhudi za kivita za Ukraine.

Hii ni kwa mujibu wa shirika la habari la Korea Kusini la Yonhap ambalo lilinukuu vyanzo vingine vya habari ambavyo halikuvitaja.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *