Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, amefanya ziara katika kaunti ya Baringo kukadiria hali ya usalama katika eneo hilo ambalo hughubikwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya majangili.
Ziara hiyo ya Murkomen inajiri kufuatia mauaji ya watu wanne katika barabara ya Marigat-Chemolingot, katika kisa cha hivi karibuni cha shambulizi la majangili kuripotiwa katika eneo hilo.
Wawili waliouawa walikuwa madereva waliokuwa wakielekea katika soko la Nginyang, huku wawili wakiwa wasafiri walioshambuliwa katika eneo la Moinonin walipokuwa wakielekea Marigat.
Visa hivyo viwili vimesababisha hali ya taharuki katika eneo hilo, huku shughuli za kiuchumi zikiathiriwa katika barabara ya Loruk – Marigat.
Wakazi wa eneo hilo wana matumaini ya utulivu na usalama kutokana na ziara hiyo ya waziri Murkomen.
Waziri huyo ameandamana na Naibu Inspekta Jenerali wa polisi Eliud Lagat, mwenzake Gilbert Masengeli, Kamanda wa kitengo cha kukabiliana na wizi w mifugo Joseph Limo, Mrakibu wa eneo la Rift Valley Dkt. Abdi Hassan, na kamanda wa polisi eneo la Rift Valley Ombati miongoni mwa maafisa wengine wakuu wa usalama.