Waziri Machogu alaani visa vya vurugu Kisii

Martin Mwanje
1 Min Read
Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu amelaani visa vya hivi karibuni vya uzushaji wa vurugu katika eneo la Kisii, akisema serikali ina rasilimali zinazohitajika kukabiliana na visa kama hivyo. 
Matamshi yake yanakuja siku chache baada ya vijana kuzua vurugu kwa kumzomea alipokuwa akisoma hotuba ya rambirambi ya Rais William Ruto wakati wa hafla ya mazishi ya mwalimu mkuu wa chuo cha kitaifa cha anuai cha Kisii Daniel Nyariki.
Akizungumza katika wadi ya Gesusu, eneo bunge la Nyaribari Masaba, Machogu aliwalaani baadhi ya wanasiasa kwa kuunga mkono vurugu kimkakati, wakati ambapo umoja miongoni mwa jamii ni muhimu mno.
Kwa upande wake, Naibu Gavana wa Kisii Robert Monda aliomba msamaha kwa madai ya kuchochewa kwa vurugu. Hii ilitokana na kisa cha hivi karibuni ambapo vijana walivuruga hafla hiyo ya mazishi iliyohudhuriwa na Waziri Machogu na Gavana wa kaunti ya Kisii Simba Arati.
Mbunge wa Imenti Kusini Shadrack Ithinji alisisitiza umuhimu wa umoja miongoni mwa viongozi wa Kisii bila kujali mirengo yao ya kisiasa ili kukuza maendeleo katika eneo hilo.
Share This Article