Waziri wa Usalama wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki ametoa onyo kali kwa wezi wa mifugo na wahalifu wanaowahangaisha Wakenya katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Amesema serikali ya Kenya Kwanza imeweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na wahalifu kupitia upelekwaji wa vikosi maalum vya usalama katika maeneo yanayokumbwa na ukosefu wa usalama.
“Wezi sugu wa mifugo na wahalifu ambao kwa miaka mingi wamewahangaisha wakazi wasiokuwa na hatia na kuwashambulia maafisa wa usalama kwa kutumia silaha haramu katika kaunti za Mashariki na Kaskazini wa Bonde la Ufa wanasakwa na vikosi vyetu maalum vya usalama,” amesema Waziri Kindiki.
“Nataka kuwaambia kuwa tuna mipango ya kukabiliana nao bila chembe ya huruma. Tutawapa tiketi moja ya kutokomea jehanamu milele.”
Waziri Kindiki alisema vikosi maalum vya usalama vitapewa silaha za kisasa kuimarisha uwezo wake wa kukabiliana na uhalifu.
Aliyazungumza hayo akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa kituo cha polisi cha Mandongoi kilichomalizwa tu kujengwa.
Maafisa wa GSU watapelekwa kuhudumu katika kituo hicho kilichopo wadi ya Ngomeni katika kata ndogo ya Mwingi Kaskazini.
Eneo hilo ni miongoni mwa wadi nane zilizo kwenye mpaka wa Kitui-Tana River na ambazo wakazi wake wamehangaishwa kwa muda mrefu na wezi wa mifugo waliojihami kwa silaha wanaovamia mashamba yao.
Migogoro ya mara kwa mara ya kupigania lishe na maji imesababisha vifo vya makumi ya wakazi wa Kitui na wengine kulemazwa. Kwa upande mwingine, mamia ya familia zimeachwa bila makazi.
Serikali ya kaunti ya Kitui chini ya uongozi wa Gavana Dkt. Julius Malombe imeahidi kushirikiana na serikali ya kitaifa kuhakikisha usalama wa wakazi wa kaunti hiyo.