Waziri wa usalama wa taifa Prof. Kithure Kindiki, amekashifu ghasia zilizoshuhudiwa katika eneo la Sondu kwenye mpaka wa kaunti za Kericho na Kisumu.
Kindiki alisema tofauti zozote ziwe za kijamii, kisiasa au kidini zinaweza kutatuliwa kwa amani na kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa waziri Kindiki, ghasia hizo zilipangwa na wahalifu kwa kisingizio cha migogoro ya mipaka na kuonya kwamba vitendo vyao havitakubalika.
Kindiki alisema hayo siku ya Jumamosi, katika soko la Sondu muda mfupi baada ya kufanya mkutano wa usalama na maafisa wa usalama na ujasusi kutoka kaunti za Kericho na Kisumu.
Waziri alisema serikali iko tayari kuwezesha juhudi za amani baina ya jamii zinazoishi kwenye miji ya mipakani kote nchini.
Mnamo Ijumaa, waziri Kindiki alizindua kambi ya maafisa wa polisi wa GSU katika mpaka wa Nkararo-Enoosaen eneo la Kilgoris kufuatia ghasia zinazochangiwa na uhasama wa kijamii kuhusu mipaka.