Waziri wa Habari, Teknolojia ya Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali William Kabogo, amewateua tena waliokuwa wanakamati 4 wa bodi ya Baraza la Vyombo vya Habari MCK kuendelea kuhudumu katika bodi hiyo na kutangaza nafasi zingine 4 kuwa wazi.
Kupitia gazeti rasmi la serikali, waziri amewateua tena Joseph Maina Muiruri kama mwenyekiti pamoja na Susan Karago, Timothy Wanyonyi Chetambe na Tabitha Mutemi ambao wameteuliwa kwa mara ya pili kama wanachama.
Wanne hao watahudumu katika bodi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Julai,25,2025.
Kwenye arifa tofauti, waziri alitangaza uwepo wa nafasi wazi 4 katika bodi hiyo na kuwataka wakenya waliohitimu kutuma maombi ya nafasi hizo katika muda wa siku 7 zijazo.
Barua za maombi zinapaswa kutumwa kwa kamati ya uteuzi kama ilivyoratibishwa katika kifungu cha 7 sehemu ya (2)b ya sheria ya vyombo vya habari.
Aidha notisi ya gazeti rasmi la serikali nambari 658 ya mwaka 2023 na nambari 1570 ya mwaka 2023 zimefutiliwa mbali.