Waziri Deborah Barasa aongoza upanzi wa miti Pokot Magharibi

Tom Mathinji
2 Min Read
Waziri Deborah Barasa aongoza upanzi wa miti Pokot Magharibi.

Waziri wa Afya anayeondoka Dkt. Deborah Barasa, leo Ijumaa aliongoza zoezi la upanzi wa miti katika kaunti ya Pokot Magharibi, katika juhudi za kupiga jeki lengo la serikali la upanzi wa miti bilioni 15, kufikia mwaka 2032.

Akizungumza Ijumaa katika msitu wa Lomukee, kaunti ndogo ya Pokot, Barasa  ambaye sasa ameteuliwa kuwa waziri wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabia Nchi na Misitu,   alielezea umuhimu wa kukumbatia mikakati ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi.

Waziri huyo alitoa wito kwa vijana kutekeleza shughuli za utunzaji wa mazingira, huku akiwahimiza wakulima kupanda miti pamoja na mimea, huku wafugaji wakitakiwa kulinda miti changa dhidi ya uharibifu wa mifugo wao..

Aliwapongeza wazee wa eneo hilo kwa kuhifadhi ukingo wa mito, hatua ambayo imeimarisha mfumo ikolojia na afya ya umma.

Alitambua kuwa eneo la Pokot Magharibi limekabiliwa na changamoto za kimazingira, ikiwa ni pamoja na ukame wa muda mrefu na uharibifu wa ardhi, akielezea dharura iliyopo wa upanzi wa miti kuhakikisha eneo hilo linapata mifumo dhabiti ya hali ya anga.

Kwa upande wake afisa mkuu wa maji na mazingira wa kaunti ndogo ya Pokot Leonard Kamsait, aliunga mkono matamshi ya Barasa, huku akitoa wito kwa jamii hiyo kupanda miti ya matunda na ile ya kiasili ambayo itawawezesha kupata mapato na kuimarisha maisha yao.

Website |  + posts
Share This Article