Wawakilishi wadi wa bunge la kaunti ya Isiolo (MCAs) wamelaani vikali shambulizi lililofanywa dhidi ya ofisi za serikali ya kaunti na ukumbi wa bunge la kaunti jana Jumatano, na wametoa wito wa utulivu na kutatuliwa kwa haraka kwa mzozo wa uongozi unaoendelea ili kuhakikisha kuwa amani inadumishwa na utoaji wa huduma kwa wakazi wa Isiolo hauathiriki zaidi.
Wakizungumza katika wadi ya Oldonyiro ambako bunge hilo limehamishia shughuli zake hadi mwezi Desemba kupisha ukarabati wa ukumbi wa bunge ulioharibiwa kwa kiwango kikubwa, viongozi hao wakiongozwa na Naibu Spika David Lemantile na kiongozi wa wengi Abdirashid Ali Diba walitaja kuchomwa kwa Ofisi ya Katibu wa Kaunti pamoja na uharibifu wa Ofisi ya Naibu Gavana na Ukumbi wa Bunge kuwa ni kitendo cha kishenzi ambacho hakiwezi kuvumiliwa katika jamii ya kisasa.
Waliitaka Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI kuchunguza kwa haraka na kufichua wote waliohusika katika uhalifu huo ili wachukuliwe hatua kali za kisheria kama funzo kwa wengine wanaoweza kufikiria kutenda uhalifu wa aina hiyo siku zijazo.
Lemantile aliwahimiza wananchi wawe waangalifu wasitumiwe kufanya uhalifu kama uharibifu wa mali, akisema kuwa ni wananchi wa Isiolo ndio watakaoumia kutokana na matokeo ya vitendo hivyo vya kihalifu kwani ni fedha za umma ambazo zingetumika kwa miradi mingine ya maendeleo zitakazotumika kukarabati ofisi na ukumbi wa bunge ulioharibiwa.
Aidha, aliwataka MCAs ambao bado wanaegemea upande wa Spika Mohamed Roba Qoto, ambaye aliondolewa katika wadhifa wake kwa njia ya utata na nafasi yake kuchukuliwa na Abdullahi Banticha Jaldesa (ambaye amepeleka kesi mahakamani kupinga kuondolewa kwake), wajiunge na wenzao huko Oldonyiro wakati vikao vya bunge vitakaporejelewa Jumanne ijayo, ili wafanye kazi kama bunge moja kwa manufaa ya wananchi wa Isiolo badala ya hali ya sasa ambapo bunge limegawanyika katika makundi mawili.
Kiongozi wa wengi na mwakilishi wa wadi ya Garbatula, Abdirashid Diba Ali, alisema kuwa MCAs ambao bado hawajahudhuria vikao vya bunge huko Oldonyiro, licha ya uhamisho wa bunge hilo kutangazwa rasmi kupitia taarifa ya gazeti rasmi la serikali tarehe 15 Agosti 2025, wanatumika kutetea maslahi ya mtu binafsi badala ya kufuata sheria na kushiriki katika shughuli halali za Bunge kwa manufaa ya wananchi waliowachagua.
Wakazi wa wadi ya Oldonyiro walifurahishwa na kufanyika kwa vikao vya bunge la kaunti katika eneo lao kwa mara ya kwanza. Victorina Edapal kutoka kambi ya juu na Esukut Lerete kutoka kijiji cha Raap walieleza kuwa hata uchumi wa eneo hilo umeimarika kwa kiasi kikubwa kutokana na ujio wa MCAs na wafanyakazi wa bunge ambao sasa wanalala, kula na kufanya manunuzi yao sokoni Oldonyiro.
Bunge linatarajiwa kusalia Oldonyiro hadi Desemba mwaka huu ambapo linatarajiwa kurejea katika ukumbi wa Isiolo mara baada ya ukarabati kukamilika.