Wawakilishi kadhaa wa Wizara ya Maji na serikali ya Kenya wako nchini Italia kutafuta suluhisho la kukamilisha miradi iliyokwama ya mabwawa.
Kundi hilo linajumuisha Waziri wa Mambo ya Nje Dkt. Alfred Mutua, Katibu wa Maji na Usafi Paul Rono na Wakili Mkuu wa serikali Shadrack Mose.
Rono alichapisha picha kwenye mtandao wa X ambayo inaonyesha walipokutana na viongozi kutoka kwa serikali ya Italia jijini Roma.
Alisisitiza kujitolea kwa serikali ya Kenya kukamilisha ujenzi wa mabwawa ya Itare, Arror na Kimwarer.
Miradi hiyo inadhamiriwa kutoa maji yatakayotumiwa nyumbani na wakazi wa maeneo hayo, wayatumie kunyunyizia mashamba na yatumike pia viwandani.
Rono aliongeza kuwa serikali ya Italia imekubali kushirikiana na serikali ya Kenya kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto zilizokumba miradi hiyo na kuhakikisha wakandarasi wanarejea na kuikamilisha.
Mwezi Machi mwaka huu katika ikulu ya Nairobi, Rais William Ruto na Rais Sergio Mattarela wa Italia walitangaza kwamba nchi hizo mbili zimekubali kuondoa kesi zote zilizowekwa mahakamani kuhusu miradi hiyo mitatu.
Kampuni za Italia zilizokuwa zimepatiwa zabuni ya ujenzi wa mabwawa hayo ziliishtaki Kenya katika mahakama ya kimataifa ya kusuluhisha mizozo zikitaka kulipwa fidia kufuatia kukwamishwa kwa miradi hiyo.