Wanasheria Tanzania wataka Tundu Lissu aachiliwe huru

Kulingana nao kukamatwa kwa Lissu ambaye pia ni wakili kitaaluma,kunadhoofisha heshima ya taaluma ya sheria na misingi ya haki.

Marion Bosire
2 Min Read
Tundu Lissu, Kiongozi CHADEMA

Chama cha Wanasheria wa Tanganyika – TLS, sasa kinataka mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha CHADEMA Tundu Lissu aachiliwe huru bila masharti yoyote.

Kulingana na chama hicho cha Tanganyika Law Society,  kukamatwa kwa Lissu ambaye pia ni wakili kitaaluma,kunadhoofisha heshima ya taaluma ya sheria na misingi ya haki.

Katika taarifa iliyotolewa Aprili 12,2025 na Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwabukusi chama hicho kiliandika, “Kuendelea kushikiliwa kwake kunaashiria vitisho kwa Wanasheria na washiriki wa siasa nchini”.

Kiliendelea kusema kwamba iwapo wito wao hautazingatiwa, chama hicho kina haki ya kupendekeza kusitishwa kwa huduma za uwakilishi wa kesi za msaada wa kisheria na huduma nyingine za kisheria za kujitolea zinazotolewa na TLS na Wanachama wake.

Hatua hiyo kilisema ni njia ya amani ya kupinga vitendo vya unyanyasaji na mashtaka yenye mlengo wa kisiasa.

TLS imemtaka pia Mkurugenzi wa Mashtaka kuhakikisha kwamba mashtaka mazito kama ya uasi yanaungwa mkono na ushahidi madhubuti na hoja za kisheria.

Ilisema pia kwamba Uongozi wa kisiasa pekee hauwezi kuchukuliwa kuwa ni kitendo cha uasi kwa mujibu wa sheria zilizopo.

“Kukamatwa kwa Wanasiasa kinyume na sheria kunaweza kusababisha upinzani na machafuko, Mamlaka zinapaswa kuchukua hatua za kisheria na za tahadhari ili kudumisha amani na umoja wa kitaifa” ilisema taarifa ya TLS.

Lissu alikamatwa kwa kile kinachodaiwa kuwa uhaini kufuatia madai kwamba alichochea wananchi kuchukua hatua dhidi ya shughuli ya kupiga kura ambapo alikuwa anaendesha kampeni ya “No reforms no elections”.

Tanzania inatizamiwa kuandaa uchaguzi wa Rais na wabunge mwezi Oktoba mwaka huu wa 2025.

Website |  + posts
Share This Article