Kundi la Wagner lajiondoa nchini Mali

Tom Mathinji and BBC
1 Min Read
Kundi la wapiganaji la Wagner.

Kundi la Wagner limetangaza kujiondoa Mali kufuatia kile walichokiita “kumalizika kwa misheni yake kuu” katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Kundi la mamluki la Urusi limekuwa likishirikiana na jeshi nchini humo tangu mwaka 2021, kukabiliana na wanamgambo wa Kiislamu.

Katika ujumbe kwenye mtandao wa Telegram, Wagner ilisema “imepambana na ugaidi hatua kwa hatua na watu wa Mali”, na kuua “maelfu ya wanamgambo na makamanda wao, ambao waliwatishia raia kwa miaka mingi”.

Tangazo hilo la kujiondoa linawadia siku ambayo kumetolewa ripoti kwamba wanajeshi wa Mali walikuwa wameondoka katika kambi kubwa katikati mwa nchi, baada ya kushambuliwa kwa mara ya pili katika muda wa chini ya wiki moja.

Mali imekuwa ikikabiliana na wanamgambo wa waasi wa Kiislamu kwa zaidi ya muongo mmoja.

Wanajeshi wa Ufaransa, ambao awali walitumwa kusaidia serikali ya kiraia, waliondoka nchini humo mwaka wa 2022.

Kufikia wakati huo, jeshi linalosimamia Mali lilikuwa tayari limeanza kufanya kazi na mamluki wa Kirusi kupambana na wanamgambo.

Mashambulizi ya wanajihadi yamekuwa yakiongezeka kwenye kambi za kijeshi katika jimbo la Sahel katika wiki za hivi karibuni.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article