Wauguzi wa kaunti ya Meru kugoma kuanzia Jumatatu

Marion Bosire
1 Min Read

Chama cha wauguzi nchini KNUN tawi la kaunti ya Meru, kimethibitisha kwamba wauguzi wa kaunti hiyo watagoma kuanzia Jumatatu Novemba 13, baada ya makataa ya siku 14  waliyotoa kwa serikali kukamilika. 

Wauguzi hao waliipa serikali ya kaunti ya Meru muda wa siku 14, ibadilishe mazingira yao ya kikazi na kuwapandisha vyeo la sivyo wagome.

Wanasema wengine wao wamekuwa kwenye kiwango kimoja cha utendakazi kwa muda wa miaka 10 sasa bila kupandishwa vyeo.

Chama hicho cha wauguzi kinasema serikali ya kaunti ya Meru haijafanya lolote kushughulikia malalamishi yao.

Sasa wauguzi hao wanasema kwamba sharti lao la msingi la kurejea kazini ni kuboreshwa kwa masharti ya kikazi na kupandishwa vyeo.

Wamejuza umma kutafuta huduma za wauguzi kwenye hospitali zisizo za umma kuanzia Jumatatu na kwamba Jumanne wataandamana hadi kwenye afisi za serikali ya kaunti ya Meru kuwasilisha malalamishi yao kwa Gavana.

Wanalalamika pia kwamba hospitali nyingi za umma za kiwango cha levels 2 na level 3 zina muuguzi mmoja huku hospitali kuu ya mafunzo na rufaa ya Meru ikiwa na wauguzi wachache ambapo muuguzi mmoja anahudumia wagonjwa zaidi ya 50 kwa wakati mmoja.

Share This Article