Watumishi wa umma waonywa dhidi ya ufisadi

Martin Mwanje
2 Min Read
Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei.

Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei amesema watumishi wa umma watawajibishwa kwa ubadhirifu wa rasilimali za umma katika idara zao.

Koskei amesema serikali inakusudia kutokomeza ufisadi na utumiaji mbaya wa rasilimali za umma.

Amewataka watumishi wa umma kusimama imara dhidi ya maelekezo yasiyokuwa halali yenye dhamira ya kuchochea cheche za ufisadi.

“Tuna wajibu wa kuokoa nchi yetu kutoka kwenye minyororo ya ufisadi,” alisema Koskei.

“Tunataka huu kuwa utawala ambao utaangamiza ufisadi katika utumishi wa umma.”

Koskei alitoa kauli hizo wakati wa mkutano wa ushauri wa wakuu wa utawala, fedha, uhasibu, usimamizi wa mfumo wa usambazaji na ukaguzi wa ndani uliofanyika katika Shule ya Serikali Nchini katika eneo la Kabete, kaunti ya Kiambu.

Alisisitiza azimio la Rais William Ruto kuongoza vita vikali na endelevu dhidi ya ufisadi akiutaja kuwa tishio kubwa kwa ustawi wa nchi.

Kadhalika Koskei aliwatahadharisha watumishi wa umma dhidi ya kuhusika katika biashara na serikali akiongeza kuwa wanapaswa kuchagua kati ya biashara na utumishi wa umma.

Alisema serikali itatumia utangazaji wa mali kutathmini mitindo ya maisha ya watumishi wa umma.

“Mitindo ya maisha isiyoendana na mali iliyotangazwa itavutia mwingilio wa mashirika yaliyotwikwa jukumu la kuzuia ufisadi na utekelezaji wa sheria,” alisema Koskei.

Kulingana naye, serikali itasimama na watumishi wa umma wanaoendeleza vita dhidi ya ufisadi.

“Hakuna atakayenyanyaswa kwa kufanya kitu kinachostahili.”

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *