Meg Whitman ajiuzulu kama Balozi wa Marekani nchini Kenya

Martin Mwanje
2 Min Read
Meg Whitman - Balozi wa Marekani anayeondoka

Balozi wa Marekani nchini Kenya Meg Whitman amejiuzulu. 

Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya baadhi ya Wakenya kushinikiza kuondolewa kwake kwenye wadhifa huo baada ya Donad Trump kushinda uchaguzi wa urais wa Marekani ulioandaliwa Novemba 5.

“Leo, naitangazia timu yangu kwenye Ubalozi wa Marekani kuwa niliwasilisha barua yangu ya kujiuzulu kwa Rais Biden. Imekuwa ni heshima kuwahudumia watu wa Marekani kupitia kuimarisha ushirikiano wetu na Kenya,” amesema Whitman katika taarifa ya kutangaza kujiuzulu kwake.

“Najivunia kuongoza ajenda iliyojikita kwa watu ambayo inaokoa maisha, kuongeza usalama na kubuni nafasi za kiuchumi kwa Wakenya na Wamarekani.”

Whitman ametaja utoaji wa fedha za dharura kukabiliana na mafuriko ya mwaka 2023, mapambano yanayoendelea dhidi ya ugonjwa wa malaria, Ukimwi na Mpox kuwa ushahidi tosha kuwa Marekani inatoa kipaumbele kwa afya na ustawi wa Kenya.

Hususan, Balozi huyo anayeondoka ametaja hatua yake ya kujiuzulu kuwa iliyotokana na uchaguzi wa urais uliofanyika nchini mwake siku chache zilizopita.

“Kama mabalozi wote wa Marekani, nahudumu kufuatia ombi la Rais. Watu wa Marekani wamezungumza na Rais mpya ataapishwa mwezi Januari. Namtakia yeye na timu yake mpya mafanikio,” alisema Whitman katika taarifa iliyoelezea baadhi ya mafanikio yake wakati wa kipindi chake cha kuhudumu.

Rais mteule wa Marekani Donald Trump ataapishwa Januari 20 mwakani, na ilikuwa wazi kwamba angemteua Balozi mwingine kuchukua nafasi ya Whitman kutokana na mirengo tofauti ya kisiasa wanayoegemea.

Whitman aliteuliwa kuhudumu kama Balozi wa Marekani nchini Kenya na Rais Joe Biden wa chama cha Democrat wakati Trump ni wa kutoka chama cha Conservative kilichovuna ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu wa Novemba 5.

Share This Article