Watu wawili wafariki baada ya basi kushambuliwa Samburu

Tom Mathinji
1 Min Read
Watu wawili wafariki baada ya basi kushambuliwa na majambazi Samburu.

Watu wawili walipigwa risasi na kufariki, huku wengine sita wakijeruhiwa Alhamisi, baada ya majambazi waliokuwa wamejihami, kushambulia basi kwenye barabara ya  Maralal-Baragoi, kaunti ya Samburu.

Kulingana na walioshuhudia, majambazi hao waliwaua utingo wawili papo hapo na kuwajeruhi abiria sita ambao wanapokea matibabu katika hospitali ya rufaa ya Maralal.

Majambazi hao walilizuia basi hilo na kuanza kulimiminia risasi, na kuanza kuwapora abiria bidhaa zao kabla ya kutorokea katika msitu uliokuwa karibu.

Viongozi wa eneo hilo wamelaani shambulizi hilo, wakitoa wito kwa serikali kuchukua hatua za dharura kukabiliana na ukosefu wa usalama katika eneo hilo.

Mbunge wa Baragoi Elly Letipila, alitaka serikali kutekeleza mikakati ya kukabiliana na mashambulizi ya majambazi hao katika eneo hilo.

Barabara kuu ya Maralal-Baragoi ni hatari kutokana na mashambulizi ya majambazi, tukio la awali likiwa mauaji ya mwakilisi wadi ya Morinjo mwaka uliopita, na shambulizi la hivi majuzi dhidi ya gari la polisi, ambapo afisa mmoja wa polisi aliuawa.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *