Wizara ya afya nchini Tanzania imethibitsha kuwa watu wawili wameambukizwa ugonjwa wa Mpox.
Waziri wa Afya nchini humo kupitia kwa taarifa, alisema watu wawili walioshukiwa kuwa na ugonjwa huo, walitengwa na kufanyiwa uchunguzi, kabla ya kubainika wanaugua ugonjwa huo.
“Mmoja wa waathiriwa hao ni dereva wa magari ya mizigo aliyetoka nchi jirani kuelekea Dar es salaam. Sampuli zilichukuliwa na kupelekwa kwa Maabara ya Taifa kwa uchunguzi,” alisema waziri huyo.
Kulingana na waziri huyo, wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais na vituo vyote vya huduma ya afya nchini humo, inatekeleza ufuatiliaji, uchunguzi na utambuzi kubaini kama kuna waathiriwa wengine wa virusi hivyo ili wapate matibabu.
“Serikali inaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa katika ngazi zote, upimaji wa wanaoingia na kutoka hapa nchini, pamoja na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kujiepusha na ugonjwa huo,” aliongeza waziri huyo.
Aliwahakikishia raia wa nchi hiyo kwamba, serikali imejitolea kukabiliana na ueneaji wa ugonjwa huo.