Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, amesema watu watano wameandikisha taarifa kwa polisi kuhusu madai ya kutekwa nyara kwa mbunge wa Juja George Koimburi.
Aidha, kulingana na Kanja maafisa wa polisi walikuwa na wakati mgumu kumfikia mbunge huyo anayepokea matibabu katika hospitali ya Karen, baada ya maafisa wa upelelezi kuzuiwa kuingia alikolazwa.
Mbunge huyo alipatikana katika shamba la kahawa, baada ya kudaiwa kutekwa nyara siku ya Jumapili baada ya kuhudhuria ibada ya kanisani.
Kanja aliyasema hayo huku kukiwa na shinikizo kutoka kwa wabunge wakitaka madai ya kutekwa nyara kwa mbunge huyu kuchunguzwa kikamilifu.
Alisema watu zaidi wanatarajiwa kuandikisha ushahidi kuhusia na madai ya kutekwa nyara kwa Koimburi, akiwemo mbunge huyo.
“Tutamhoji punde tu tutakapopata nafasi, familia yake ilizui juhudi zetu za kutaka kumfikia,” alisema Kanja.
Aliwahakikishia wakenya kwamba Huduma ya Taifa ya Polisi itajizatiti kuhakikisha ukweli unabainika kuhusu madai hayo.