Watu wanne wafariki katika mkanyagano uliotokea Kericho Green

Tom Mathinji
1 Min Read
Uwanja wa michezo wa Kericho Green.

Watu wanne wamefariki na wengine 13 kujeruhiwa Ijumaa asubuhi, baada ya kutokea kwa mkanyagano wa watu katika uwanja wa michezo Kericho Green.

Kulingana na ripoti ya polisi, mkanyagano huo ulisababishwa na mchuuzi wa chai majira ya alfajiri, wakati chai ilipomwagika kwenye moto na kusababisha moshi uliodhaniwa kuwa kitoza machozi.

Polisi walisema kuwa watu tisa walipata majeraha mabaya, huku wanne wakiwa na majeraha madogo, na wanapokea matibabu katika hospitali ya rufaa ya kericho.

“Watu kadhaa waliokuwa wakiingia katika uwanja wa Kericho Green, walijeruhiwa na kupelekwa katika hospitali ya rufaa ya Kericho,” ilisema ripoti ya polisi.

Aidha ripoti hiyo ya polisi ilisema kuwa miili ya waliofariki ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya rufaa ya Kericho, ikisubiri upasuaji.

Kulingana na waziri wa michezo Ababu Namwamba, uwanja wa Kericho Green una uwezo wa kuwa na watu 10,000.

Siku kuu ya Mashujaa huandaliwa kila mwaka kuwakumbuka Mashujaa waliopigania uhuru wa taifa hili.

Share This Article