Takriban watu sita wamefariki katika mkasa wa moto uliotokea usiku wa Novemba 19,2024 katika kijiji cha Kitui, eneo la Majengo, Pumwani kaunti ya Nairobi.
Kulingana na ripoti watu wengine 16 walipata majeraha wakati wa mkasa huo, huku wakipelekwa kupokea matibabu katika vituo vya afya vilivyo karibu.
Shirika la msalaba mwekundu kupitia ukurasa wake wa X, lilisema zaidi ya nyumba hamsini ziliteketezwa, familia nyingi zikiachwa bila makao.
“Takriban nyumba 50 ziliteketezwa na moto huo,” lilisema shirika hilo.
Shirika hilo la Msalaba Mwekundu lilisema, lilishirikiana na wananchi kukabiliana na kuuzima moto huo, ambao chanzo chake hakijabainishwa.
Mkasa huo umesababisa hasara kubwa kwa familia nyingi huku waathiriwa wakitoa wito wa kusaidiwa kujenga upya makazi yao.