Watu 90 wafariki katika mkasa wa Feri Msumbiji

Tom Mathinji
1 Min Read

Zaidi ya watu 90 wamefariki baada ya feri kuzama katika pwani ya kaskazini mwa Msumbiji, mamlaka za eneo zilisema.

Maafisa katika jimbo la Nampula walisema watu watano wameokolewa kati ya watu 130 wanaoaminika kuwa ndani ya feri hiyo.

Walikuwa wakikimbia mlipuko wa kipindupindu, katibu wa jimbo la Nampula Jaime Neto alisema. Watoto wengi ni miongoni mwa waliofariki, aliongeza.

“Kwa sababu feri hiyo ilikuwa imejaa watu wengi na haikufaa kubeba abiria iliishia kuzama,” Bw Neto alisema.

Video ambayo haijathibitishwa iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii inadaiwa kuonyesha makumi ya miili ikiwa imelala ufukweni.

Feri hiyo inaonekana ilikuwa ikisafiri kutoka Lunga kuelekea kisiwa cha Msumbiji, nje ya pwani ya Nampula.

Mkoa wa Nampula umekuwa miongoni mwa sehemu zilizoathiriwa zaidi na ugonjwa wa kipindupindu ambao umeenea katika mataifa kadhaa kusini mwa Afrika tangu Januari mwaka jana.

Kulingana na Unicef, mlipuko wa sasa ndio mbaya zaidi katika miaka 25. Tangu Oktoba 2023, Msumbiji imeripoti visa 13,700 vilizothibitishwa na vifo 30.

TAGGED:
Share This Article