Angalau watu 64 wameangamia kwenye vurugu za kikabila katika nyanda za juu za eneo la kaskazini mwa nchi ya Papua New Guinea.
Afisa mmoja wa polisi alitaja mauaji hayo kuwa makubwa zaidi kuwahi kutokea katika taifa hilo katika miaka ya hivi karibuni.
Vurugu hizo kati ya makabila ya Ambulin na Sikin zinaripotiwa kuanza Jumapili Februari 18 alfajiri katika wilaya ya Wapenamanda mkoa wa Enga.
Polisi waliambia wanahabari kwamba waliondoa miili 64 katika eneo la tukio kando kando ya barabara Jumatatu asubuhi.
Wahusika wa vita hivyo wanasemekana kutumia bunduki za nguvu kama AK47 na M4, huku idadi ya vifo ikitarajiwa kuongezeka.
Shirika la utangazaji la Australia, ABC liliripoti kwamba makabila yanayozozana sasa ndiyo yalizozana mwaka jana ambapo vifo zaidi ya 60 viliripotiwa.
George Kakas, afisa wa ngazi za juu katika huduma ya polisi nchini Papua New Guinea anasema wamesikitishwa na vurugu hizo.
Wanajeshi wapatao 100 wametumwa katika eneo hilo lakini wamezidiwa na wapiganaji ambao ni wengi na wana silaha nyingi.
Katika jiji kuu Port Moresby, wapinzani wa serikali ya waziri mkuu James Mara waliozungumza na wanahabari waliitisha maafisa zaidi wa usalama.
Wanataka serikali itambue zinakotoka silaha ambazo raia wanatumia kwenye vurugu hizo za kikabila.
Waziri mkuu wa Australia Anthony Albanese naye ameelezea wasiwasi kuhusu hali hiyo akiahidi kutoa usaidizi unaohitajika hasa utoaji wa mafunzo kwa maafisa wa usalama wa Papua New Guinea.