Watu 422 wameorodheshwa na upande wa mashtaka kutoa ushaidi dhidi ya mhubiri tata Paul Mackenzie, anayekabiliwa na mashtaka 238 ya mauaji bila kukusudia pamoja na washukiwa wengine 94, wakati kesi hiyo ilipoanza kusikilizwa rasmi Jana Jumatatu.
Mashahidi hao, wanajumuisha 13 ambao wako chini ya mpango wa ulinzi wa mashahidi, wanatarajiwa kuelezea kinaga ubaga kilichotokea katika msitu wa Shakahola, huku upande wa mashtaka ukitaja tukio hilo kuwa baya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika sekta ya dini hapa nchini.
Walipofikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Alex Ithuku katika mahakama moja ya Mombasa jana Jumatatu, washukiwa hao walikanusha mashtaka dhidi yao.
Hakimu Thuku alifahamishwa kwamba kando na ushahidi wa mashahidi hao, ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP, pia itawasilisha ushahidi wa kielektroniki na ushahidi mwingine wa kuthibitisha kesi hiyo.
Jaji huyo alifahamishwa kuwa miili 429 ya wanaume, wanawake na watoto waliosusia chakula hadi kufa, ilipatikana katika makaburi kwenye msitu huo, lililoko katika eneo la Langobaya, kaunti ndogo ya Malindi.
Kesi hiyo itaendelea kila siku mfululizo ili kuzipa haki pande zote husika akiwemo Mackenzie na washtakiwa wenza ambao wamenyimwa dhamana.
Mauaji ya Shakahola ambayo yalilishangaza taifa yanadaiwa kutekelezwa kati ya mwezi Januari mwaka 2021 na mwezi septemba mwaka 2023 katika sehemu ya Shakahola, kaunti ndogo ya Malindi kaunti ya Kilifi.