Watu wanne wamefariki katika ajali ya barabarani iliyotokea mapema leo Jumatatu alfajiri eneo la Hill Tea kwenye barabara ya Eldoret-Nakuru.
Ajali hiyo iliyotokea majira ya saa kumi na moja, ilihusisha matatu moja iliyokuwa ikielekea mjini Nakuru na basi.
Kulingana na Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS, ajali hiyo ilitokea baada ya dereva wa matatu hiyo inayomilikiwa na kampuni ya Msamaria Shuttle Ltd kushindwa kuidhibiti na hivyo kugongana ana kwa ana na basi hilo la abiria 60.
Matatu hiyo ilikuwa imebeba abiria 16 wakati wa ajali hiyo iliyosababisha vifo vya dereva wake na abiria wengine watatu waliofariki papo hapo.
Abiria wengine 9 walijeruhiwa vibaya na kwa sasa wanatibitiwa katika hospitali ya rufaa ya kaunti ndogo ya Eldama Ravine.
NPS inatoa wito kwa waendeshaji magari na watumiaji wengine wa barabara kuwa waangalifu zaidi wanapokuwa barabarani hasa msimu huu wa mvua.