Watu wapatao 35 wanahofiwa kufariki kufuatia shambulizi la droni, linalodaiwa kutekelezwa na jeshi la Sudan wakati wa kikao cha baraza la wazee kaskazini mwa Darfur.
Kulingana na Kundi la Mawakili la Emergency Lawyers Group, watu wengine kadhaa walijeruhiwa kwenye shambulizi hilo lililotokea juzi Jumapili alasiri.
Shirika hilo limesema shambulizi hilo lilitokea katika kijiji cha Ghara al-Zawiya, kinachodhibitiwa na kikosi cha Rapid Support Forces (RSF), wakati wananchi walikusanyika mahakamani kusikiliza utatuzi wa kesi za eneo hilo.
Shambulizi hilo pia liliharibu jengo la mahakama ambalo limekuwa likitumika kutatua mizozo katika eneo hilo.
Kulingana na shahidi mmoja, vikao vya kusikiliza kesi havikuwa ndani ya jengo hilo, lakini vilifanywa nje chini ya mti na kuhudhuriwa na wazee wa jamii hiyo.
Alidokeza kuwa waliofariki kwenye shambulizi hilo ni pamoja na viongozi wanne wa jamii hiyo na makamanda wawili wa RSF.
Kundi la RSF linadhibiti sehemu kubwa ya eneo la Darfur, magharibi mwa Sudan, huku mapigano kati yake na jeshi la Sudan yakiendelea katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitatu.
Vita hivyo vimeharibu sehemu kubwa ya nchi hiyo, vimesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwalazimu mamilioni kuyahama makazi yao.