Marekani imeendeleza mashambulizi dhidi ya Iran kwa usiku wa tisa mfululizo, huku vyombo vya habari vya Iran vikiripoti milipuko katika miji kadhaa, ikiwemo Sirik, Jask, Tabriz na Chabahar.
Mashambulizi ya Jumatatu yalijiri wakati jeshi la Marekani lilitangaza kifo cha mwanajeshi wa tatu ndani ya siku za hivi karibuni huku makubaliano ya kusitisha mapigano ya mwezi mmoja kati ya Tehran na Washington yakianza kuvunjika kutokana na mvutano wa kudhibiti Mlango-Bahari wa Hormuz.
Katika taarifa, jeshi la Marekani lilisema mashambulizi hayo ya hivi karibuni yalilenga kupunguza uwezo wa kijeshi wa Iran unaotumika kushambulia meli za kibiashara na mabaharia wanaopita katika Mlango-Bahari wa Hormuz.”
Shirika la utangazaji la serikali ya Iran, IRIB lilisema milipuko kadhaa ilisikika katika miji ya bandari ya Mahshahr na Imam Khomeini, katika jimbo la kusini-magharibi la Khuzestan.
Pia liliripoti milipuko mingine karibu na miji ya Sirik na Jask katika jimbo la Hormozgan kwenye pwani ya kusini ya Iran, pamoja na karibu na mji wa Khvormuj katika jimbo la Bushehr.
Milipuko mitatu pia ilisikika karibu na mji wa Tabriz kaskazini-magharibi mwa Iran, IRIB iliongeza. Wakati huo huo, mifumo ya ulinzi wa anga iliwashwa katika miji ya Konarak na Chabahar kusini-mashariki mwa jimbo la Sistan na Baluchestan, kwa mujibu wa shirika la habari la Fars.